Na wewe, Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani hii, na kuleni humo mpendapo. Wala msiukaribie mti huu, mkawa katika wale walio dhulumu. (19) Basi Shet'ani aliwatia wasiwasi ili kuwafichulia tupu zao walizo fichiwa, na akasema: Mola Mlezi wenu hakukukatazeni mti huu ila msije mkawa Malaika, au msije mkawa katika wanao ishi milele. (20) Naye akawaapia: Kwa yakini mimi ni miongoni wa wanao kunasihini. (21) Basi akawateka kwa khadaa. Walipo uonja ule mti, tupu zao zilifichuka na wakaingia kujibandika majani ya Bustanini. Mola wao Mlezi akawaita: Je, sikukukatazeni mti huo, na kukwambieni ya kwamba Shet'ani ni adui yenu wa dhaahiri? (22) Wakasema: Mola wetu Mlezi! tumejidhulumu nafsi zetu, na kama hutusamehe na kuturehemu, hakika tutakuwa katika wenye kukhasirika. (23) Akasema: Teremkeni! Mtakuwa nyinyi kwa nyinyi maadui. Na kwenye ardhi itakuwa ndio makao yenu na starehe yenu mpaka ufike muda. (24) Akasema: Humo mtaishi, na humo mtakufa, na kutoka humo mtatolewa. (25)