Wanafunzi walipo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Je, Mola wako Mlezi anaweza kututeremshia chakula kutoka mbinguni? Akasema: Mcheni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini. (112) Wakasema: Tunataka kukila chakula hicho, na nyoyo zetu zitue, na tujue kwamba umetuambia kweli, na tuwe miongoni mwa wanao shuhudia. (113) Akasema Isa bin Maryamu: Ewe Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wetu! Tuteremshia chakula kutoka mbinguni ili kiwe Sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni Ishara itokayo kwako. Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye mbora wa wanao ruzuku. (114) Mwenyezi Mungu akasema: Hakika Mimi nitakuteremshieni hicho. Lakini yeyote katika nyinyi atakaye kanya baadae, basi hakika Mimi nitampa adhabu nisiyopata kumpa yeyote katika walimwengu. (115)