Na Firauni akasema: Ewe Hamana! Nijengee mnara ili nipate kuzifikia njia, (36) Njia za mbinguni ili nikamwone Mungu wa Musa. Na kwa hakika mimi bila ya shaka namjua kuwa ni mwongo tu. Na hivi ndivyo Firauni alivyo pambiwa ubaya wa vitendo vyake, na akazuiliwa Njia. Na vitimbi vya Firauni havikuwa ila katika kuangamia tu. (37) Na yule aliye amini alisema: Enyi watu wangu! Nifuateni mimi, nitakuongozeni njia ya uwongozi mwema. (38) Enyi watu wangu! Hakika haya maisha ya dunia ni starehe ipitayo tu, na hakika Akhera ndiyo nyumba ya daima. (39) Mwenye kutenda uovu hatalipwa ila sawa na huo uwovu wake, na anaye tenda wema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi, waruzukiwe humo bila ya hisabu. (40) Na enyi watu wangu! Kwa nini mimi nakuiteni kwenye uwokofu, nanyi mnaniita kwenye Moto? (41) Mnaniita nimkufuru Mwenyezi Mungu na nimshirikishe na yule ambaye simjui, nami nakuiteni kwa Mwenye nguvu Mwenye kusamehe? (42) Bila ya shaka mnaye niitia kumuabudu hastahiki wito duniani wala Akhera. Na hakika marejeo yetu ni kwa Mwenyezi Mungu. Na wanao pindukia mipaka ndio watu wa Motoni! (43)