Na akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni hawa walio tumwa. (20) Wafuateni ambao hawakutakini ujira, hali ya kuwa wenyewe wameongoka. (21) NA KWA NINI nisimuabudu yule aliye niumba na kwake mtarejeshwa? (22) Je! Niishike miungu mingine badala yake? Arrahmani, Mwingi wa Rehema, akinitakia madhara uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa. (23) Basi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotovu ulio dhaahiri. (24) Hakika mimi nimemuamini Mola wenu Mlezi, basi nisikilizeni! (25) Akaambiwa: Ingia Peponi! Akasema: Laiti kuwa watu wangu wangeli jua (26) Jinsi Mola wangu Mlezi alivyo nisamehe, na akanifanya miongoni mwa walio hishimiwa. (27)