Na kwa A'adi tulimpeleka ndugu yao, Hud. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu ila Yeye. Basi je, hamumchi? (65) Wakasema watukufu wa wale walio kufuru katika kaumu yake: Sisi tunakuona umo katika upumbavu, na hakika sisi tunakufikiria kuwa wewe ni katika waongo. (66) Akasema: Enyi watu wangu! Mimi sina upumbavu. Lakini mimi ni Mtume niliye toka kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote. (67) Nakufikishieni ujumbe wa Mola wangu Mlezi. Na mimi kwenu ni mwenye kukunasihini, muaminifu. (68) Mnaona ajabu kukufikieni mawaidha yanayo toka kwa Mola wenu Mlezi kwa mtu aliye mmoja wenu nyinyi ili akuonyeni? Na kumbukeni alivyo kufanyeni mshike pahala pa kaumu ya Nuhu, na akakuzidisheni katika umbo. Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa. (69) Wakasema: Je! Umetujia ili tumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na tuyaache waliyo kuwa wakiyaabudu baba zetu? Basi tuletee hayo unayo tuahidi, ukiwa miongoni mwa wasemao kweli. (70) Akasema: Bila ya shaka adhabu na ghadhabu zimekwisha kukuangukieni kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Mnabishana nami kwa ajili ya majina tu mliyo yaita nyinyi na baba zenu ambayo kwayo Mwenyezi Mungu hakuteremsha uthibitisho? Basi ngojeni, mimi pia ni pamoja nanyi katika wanao ngoja. (71) Basi tukamwokoa yeye na walio kuwa pamoja naye kwa rehema zetu, na tukakata mizizi ya wale walio zikanusha Ishara zetu, na hawakuwa wenye kuamini. (72)