Hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryamu! Na hali Masihi mwenyewe alisema: Enyi Wana wa Israili! Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Kwani anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu atamharimishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na walio dhulumu hawatakuwa na wa kuwanusuru. (72) Kwa hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu ni wa tatu wa Utatu. Hali hakuna mungu ila Mungu Mmoja. Na ikiwa hawaachi hayo wanayo yasema, kwa yakini itawakamata adhabu chungu wale wanao kufuru. (73) Je! Hawatubu kwa Mwenyezi Mungu na wakamwomba msamaha? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu. (74) Masihi mwana wa Maryam si chochote ila ni Mtume. Wamekwisha pita Mitume kabla yake. Na mama yake ni mwanamke mkweli. Wote wawili walikuwa wakila chakula. Angalia jinsi tunavyo wabainishia Aya, kisha angalia vipi wanavyo geuzwa. (75) Sema: Je! Mnawaabudu, badala ya Mwenyezi Mungu, wale ambao hawawezi kukudhuruni wala kukufaeni? Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kujua. (76) Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu bila ya haki. Wala msifuate matamanio ya watu walio kwisha potea tangu zamani, na wakawapoteza wengi, na wenyewe wakapotea njia iliyo sawa. (77)