Na Sisi tulimtuma Nuhu kwa watu wake, akawaambia: Hakika mimi ni mwonyaji kwenu ninaye bainisha, (25) Ya kwamba msimuabudu isipo kuwa Mwenyezi Mungu tu. Hakika mimi ninakukhofieni adhabu ya Siku Chungu. (26) Na wakasema wakuu walio kufuru katika kaumu yake: Hatukuoni wewe ila ni mtu tu kama sisi, wala hatukuoni wamekufuata ila wale walio kuwa kwetu watu duni, wasio kuwa na akili. Wala hatukuoneni kuwa mna ubora wowote kutushinda sisi. Bali tuna hakika nyinyi ni waongo. (27) Akasema: Enyi watu wangu! Hebu fikirini! Ikiwa mimi ninayo hoja wazi iliyo toka kwa Mola wangu Mlezi, na amenipa rehema kutoka kwake, nayo ikakufichikieni; je, tukulazimisheni kuikubali hali nyinyi mnaichukia? (28) Na enyi watu wangu! Mimi sikuombeni mali kwa ajili ya haya. Mimi sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu; na mimi sitawafukuza walio amini. Hakika wao watakutana na Mola wao Mlezi, lakini mimi nakuoneni mnafanya ujinga. (29) Na enyi watu wangu! Ni nani atakaye nisaidia kwa Mwenyezi Mungu nikiwafukuza hawa? Basi je, hamfikiri? (30) Wala sikwambiini kuwa nina khazina za Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi najua mambo ya ghaibu; wala sisemi: Mimi ni Malaika. Wala siwasemi wale ambao yanawadharau macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri - Mwenyezi Mungu anajua yaliomo katika nafsi zao - hapo bila ya shaka ninge kuwa miongoni mwa wenye kudhulumu. (31) Wakasema: Ewe Nuhu! Umejadiliana, na umekithirisha kutujadili. Basi tuletee hayo unayo tuahidi, ukiwa miongoni mwa wasemao kweli. (32) Akasema: Mwenyezi Mungu atakuleteeni akipenda. Wala nyinyi si wenye kumshinda. (33) Wala nasaha yangu haikufaini kitu nikitaka kukunasihini, ikiwa Mwenyezi Mungu anataka kukuachieni mpotee. Yeye ndiye Mola wenu Mlezi; na kwake mtarejeshwa. (34) Au ndio wanasema: Ameizua? Sema: Ikiwa nimeizua, basi kosa hilo ni juu yangu, na mimi sikhusiki na makosa myatendayo. (35)