Hakika Qaruni alikuwa katika watu wa Musa, lakini aliwafanyia dhulma. Na tulimpa khazina ambazo funguo zake zinawatopeza watu wenye nguvu kuzichukua. Walipo mwambia watu wake: Usijigambe! Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wanao jigamba. (76) Na utafute, kwa aliyo kupa Mwenyezi Mungu, makaazi ya Akhera. Wala usisahau fungu lako la dunia. Nawe fanya wema kama Mwenyezi Mungu alivyo kufanyia wema wewe. Wala usitafute kufanya ufisadi katika ardhi. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi mafisadi. (77) Akasema: Kwa hakika nimepewa haya kwa sababu ya ilimu niliyo nayo. Je! Hakujua kwamba Mwenyezi Mungu kesha waangamiza, katika vizazi vya walio kabla yake, watu walio kuwa wenye ngubvu zaidi kuliko yeye, na wenye makundi makubwa zaidi kuliko yake. Na wakosefu hawataulizwa khabari ya dhambi zao. (78)