Na kwa Thamud tulimpeleka ndugu yao, Saleh. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika imekwisha kukufikieni Ishara iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Huyu ni ngamia jike wa Mwenyezi Mungu aliye ni Ishara kwenu. Basi mwachieni ale kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimdhuru, isije kukushukieni adhabu chungu. (73) Na kumbukeni alivyo kufanyeni wa kushika pahala pa A'adi na akakuwekeni vizuri katika nchi, mnajenga majumba ya fakhari katika nyanda zake, na mnachonga majumba katika milima. Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu wala msitende uovu katika nchi kwa ufisadi. (74) Waheshimiwa wa kaumu yake wanao jivuna waliwaambia wanao onewa wenye kuamini miongoni mwao: Je, mnaitakidi ya kwamba Saleh ametumwa na Mola Mlezi wake? Wakasema: Hakika sisi tunayaamini yale aliyo tumwa. (75) Wakasema wale wanao jivuna: Sisi tunayakataa hayo mnayo yaamini. (76) Na wakamuuwa yule ngamia, na wakaasi amri ya Mola Mlezi wao, na wakasema: Ewe Saleh! Tuletee unayo tuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume. (77) Basi tetemeko la ardhi likawanyakua, na kulipo kucha wakawa majumbani mwao kifudifudi wamekwisha kufa. (78) Basi Saleh akwaacha na akasema: Enyi watu wangu! Nilikufikishieni Ujumbe wa Mola wangu Mlezi, na nikakunasihini, lakini nyinyi hamwapendi wenye nasaha. (79)