Na alikusanyiwa Sulaiman majeshi yake ya majini, na watu, na ndege; nayo yakapangwa kwa nidhamu. (17) Mpaka walipo fika kwenye bonde la wadudu chungu, alisema mdudu chungu mmoja: Enyi wadudu chungu! Ingieni majumbani mwenu, asikupondeni Sulaiman na majeshi yake bila ya wao kutambua. (18) Basi (Sulaiman) akatabasamu akacheka kwa neno hili, na akasema: Ee Mola wangu Mlezi! Nizindue niishukuru neema yako uliyo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nipate kutenda mema uyapendayo, na uniingize kwa rehema yako katika waja wako wema. (19) Na akawakagua ndege, na akasema: Imekuwaje, mbona simwoni Hud-hud, au amekuwa miongoni mwa walio ghibu? (20) Kwa yakini nitamuadhibu kwa adhabu kali, au nitamchinja, au aniletee hoja ya kutosha. (21) Basi (Hud-hud) akakaa si mbali na akasema: Nimegundua usilo gundua wewe, na ninakujia hivi kutoka nchi ya Sabai, na nakuletea khabari za yakini. (22)