Tena Mola wake Mlezi akampokea kwa mapokeo mema na akamkuza makuzo mema, na akamfanya Zakariya awe mlezi wake. Kila mara Zakariya alipo ingia chumbani kwake alimkuta na vyakula. Basi alimwambia: Ewe Maryamu! Unavipata wapi hivi? Naye akasema: Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu. (37) Pale pale Zakariya akamwomba Mola wake Mlezi, akasema: Mola wangu Mlezi! Nipe kutoka kwako uzao mwema. Wewe ndiye unaye sikia maombi. (38) Alipo kuwa kasimama chumbani akisali, Malaika kamnadia: Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria Yahya, ataye kuwa mwenye kusadikisha neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu, na ni bwana na mt'awa na Nabii kwa watu wema. (39) Akasema Zakariya: Mola wangu Mlezi! Vipi nitapata mwana na hali ukongwe umenifikia, na mke wangu ni tasa? Akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo. (40) Akasema: Mola wangu Mlezi! Niwekee alama. Akasema: Alama yako ni kuwa hutasema na watu kwa siku tatu, isipo kuwa kwa kuashiria tu. Na mdhukuru Mola Mlezi wako kwa wingi na mtakase jioni na asubuhi. (41)